MZOZO WA UTAMBULISHO WA MAMLAKA MAKUU: MBINU YA KUONDOA UKOLONI KATIKA TEKNOLOJIA DIJITALI INAONYESHA NINI KUHUSU MZOZO WA UTAMBULISHO WA MAMLAKA MAKUU?
Volume 95, No. 4, Summer 2023
By Nanjala Nyabola [PDF]

Dhana ya “mzozo wa utambulisho wa mamlaka makuu” katika enzi ya dijitali ina dhana nyingi zinazobishwa – mamlaka makuu, utambulisho na hata enzi ya dijitali.1 Hata hivyo, ni dhahiri kwamba mzozo wa aina fulani unaounganisha masuala haya yote unaendelea. Huluki inayochukuliwa kumiliki mamlaka makuu – yaani nchi – inapingwa kwa njia mbalimbali kama vile ukinzani, mizozo na uhamaji wa watu wengi; mengi ya hayo yanaratibiwa au kukuzwa na teknolojia dijitali. Msukumo wa kuitaka mifumo ya kimataifa isuluhishe mizozo kati ya mataifa kuhusu masuala ya teknolojia dijitali yakiwemo utozaji kodi, utengenezaji, uzalendo na mengineyo, unazidi kuenea. Aina zote za utambulisho hufanywa kupitia mifumo dijitali ya utambulisho, iwe ni uraia au utambulisho wa kijinsia au wa kikabila. Bila shaka mabadiliko makubwa yanafanyika na kazi iliyopo ni kufafanua mzozo huo kwa njia inayoangazia mpango mwafaka wa hatua za kuchukuliwa na kuwapigisha wanadamu hatua mbele.

Kimsingi, ahadi ya enzi ya dijitali ilikuwa kwamba kwa kuboresha usafiri na mawasiliano, tungeweza kuwaleta watu binafsi na pia jamii karibu zaidi. Badala yake, karne ya 21 inaonekana kuwa kipindi cha kugawanyika kwingi, kinyume na ishara za maendeleo ambazo pia zinadhihirika katika kila ngazi ya jamii. Watu, jamii na mifumo zaidi sasa imeunganishwa kushinda hapo zamani, lakini kwa wengi, hali yao ya matumizi ya dijitali imegawanyika. Kwa mfano, idadi kubwa ya watu duniani hutumia intaneti kupitia tafsiri au kidhahania kwa sababu intaneti inachukulia kwamba mtumiaji wa kawaida ni mwanamume anayezungumza Kiingereza, mwenye elimu nzuri na ambaye ana nguvu nyingi sana za kisiasa nje ya mtandao kiasi kwamba kubanwa kwa haki zake dijitali mtandaoni ni ukiukaji mdogo tu wa muktadha wa haki zake kijumla. Hili linadhihirika katika idadi kubwa ya teknolojia dijitali ambazo zinapatikana kwa Kiingereza pekee, jinsi haki za wanawake zinavyodunishwa mtandaoni kila uchao na jinsi kampuni kuu za teknolojia zinavyokosa kupatia kipaumbele njia zinazozingatia haki za kubuni teknolojia. Couldry  na Mejias (2019) wanaeleza kwamba uchopoaji wa malighafi ndio kiini cha mfumo wa sasa wa kubuni na kuendeleza teknolojia na kwamba hili linasadikisha madai ya ukoloni dijitali. Kimsingi, lengo la ukoloni lilikuwa kubadilisha sehemu fulani za ulimwengu na watu walioishi au kutokea huko kuwa maeneo ya kuchopoa malighafi kwa manufaa ya maeneo mengine ya ulimwengu. Si suala la utwaaji wa data tu, bali ni utwaaji wa data “kwa masharti ambayo kwa kiasi fulani au kabisa hayawezi kudhibitiwa na mtu ambaye data hiyo inamhusu”.2

Kwa hivyo, makala hii inatoa hoja kwamba mfumo bora zaidi wa kinadharia wa kukabiliana na mzozo wa mamlaka makuu, bila kuzidisha utenganisho ambao tayari unaletwa na enzi ya dijitali katika maeneo mengi duniani, ni mfumo wa kuondoa ukoloni. Ikiangazia zaidi ya dhana pungufu kuhusu mamlaka makuu zisizotambua vya kutosha tofauti za nguvu kati ya wahusika mbalimbali wa data katika jamii tofauti, makala hii inachunguza eneo ambapo tofauti za nguvu ni kubwa zaidi na dhahiri zaidi – mpakani. Makala hii inatoa hoja kwamba siasa za kijela za mipaka ni dalili ya matumizi yaliyokithiri ya mamlaka makuu dhidi ya vikundi vilivyo hatarini sana, na pia zinapelekea mgongano kati ya nchi zinazotumia siasa hizo na dhana zilizokita za hali ya kuwa nchi na ushirikiano wa kimataifa. Hivyo, kwa kutumia mpaka kama mfano na pia eneo muhimu katika kuelewa mzozo wa mamlaka makuu, makala hii inatoa hoja kwamba mbinu ya kuondoa ukoloni katika kuelewa teknolojia dijitali inahitajika katika kukabiliana na madhara yaliyopo na yajayo kutokana na mzozo huo.